Karamu Garini
Karamu Ambayo Ingekuwa
Walikuwepo watu wengi kwenye treni kutoka Vladikavkaz hadi Mineralnye Vody. Iliendelea kusimama na kuondoka. Kusimama na kuondoka. Ilipokuwa imekaa kwenye reli, watu walianza kupoteza subira. Zaidi ya kupoteza subira, wakawa na njaa.
Mwanamke mwenye nywele nyeusi kabisa alitoa begi kubwa la machungwa madogo. Hicho ndicho tu alichokuwa nacho, lakini lazima yalikuwa angalau ishirini ndani.
Mwanaume mwenye kofia ya kijivu alitoa nusu ya gurudumu kubwa la jibini nyeupe. Hicho ndicho tu alichokuwa nacho. Hicho na kisu cha kukikatia.
Msichana mdogo aliyevaa sweta ya bluu ya kifalme alitoa mkate wa unga mweusi uliotoka okoni. Huo ndio tu alikuwa nao.
Mzee mwenye nywele za kijivu zilizovurugika na tumbo lililojaa alishika kiganja chake cha kushoto usoni, lakini akachungulia chini yake kwa jicho moja. Hakuwa na chochote isipokuwa miono yake.
Mwanamke kijana mwenye mtoto aliyevaa nguo za njano alikuwa na chupa chache za maji chini ya kigari cha mtoto. Hivyo ndivyo tu alikuwa navyo. Hivyo na mtoto wake.
"Je, kipande cha jibini hakingeendana vyema na mkate huo mweusi?" alisema mzee wa nywele zilizovurugika kwa sauti ndogo. Akidhani hakuna mtu anayemsikia.
"Hicho na chungwa dogo," alinong'ona.
Mwanaume wa kofia ya kijivu alichukua tonge lingine la jibini lenye chumvi. Alikuwa na kiu sana. "Ningehitaji funda la maji au angalau chungwa dogo," alinong'ona, akidhani hakuna mtu anayemsikia.
Mwanamke kijana mwenye mtoto alikuwa akinyonyesha. Alinusa harufu ya mkate mweusi na jibini nyeupe, akamsikia mwanamke wa nywele nyeusi nyuma yake akitafuna machungwa madogo.
Msichana wa sweta ya bluu ya kifalme alimtazama mwanaume wa kofia ya kijivu akikata jibini lake.
Treni ilianza kutembea tena kwenye reli.
Kila mmoja alikula chakula chake huku jicho moja likiwa kwenye sahani za wengine.
Mzee mwenye nywele za kijivu zilizovurugika na tumbo lililojaa aliangusha uso wake kwenye viganja vyote viwili.
Pamoja, ingekuwa karamu kiasi gani.
A story by Pemba Umoja