Sanaa ya Uchoshi
Darasa, Mzunguko, Chaguo
“Karibuni darasani. Ingieni. Ketini, au laleni sakafuni mkipenda. Mnaweza kukaa chila pia, au hata kuinyoosha miguu. Vyovyote vile inafaa. Kwa hakika, mnaweza kuketi, kulala, kusimama, au kufanya mkao mwingine. Mkao wa mwili wenu ni kama turubai wazi. Miguu yenu na mikono, kichwa, na kiwiliwili ni kama rangi kwenye kibao cha mchoraji.”
“Samahani, bwana. Samahani, mwalimu.”
“Ndiyo.”
“Utalianza darasa lini?”
“Naam, mwanangu, limeshaanza tayari.”
“Kuna viti na mabenchi kwa matumizi yenu pia. Na ile meza kule nyuma, yeyote anaweza kuitumia. Lakini tafadhali, hebu tuepuke kanyagano. Sitaki kuona mwanafunzi wangu yeyote akikanyagwa leo.”
“Loo, na isitoshe, nusura nisahau. Msisahau kupumua. Na hii ni ya ziada. Mnaweza kubadilisha mkao. Mnaelewa ninachomaanisha?”
“La,” akauliza msichana mwenye haya na nywele nyekundu, aliyekuwa amelala chali.
“Naam, unaweza, kwa mfano, kwenda mahali pengine humu chumbani, ukakunja kiungo, ukageuza kichwa. Ukasimama.”
“Na hapa ndipo penye raha. Mnaweza kufanya hivyo mara nyingi mpendavyo.”
Mzee mmoja mwenye ndevu ndefu za mvi aliinuka na kuanza kucheza dansi.
“Haha, safi sana. Mnaweza kuwa kwenye mwendo usiokoma pia.”
Yule msichana mwenye nywele nyekundu aliinuka na kuanza kuzungusha nyonga zake.
“Huna haja ya hula hoop,” akacheka mwalimu. “Safi kabisa. Mmeanza kupata sasa.”
Kisha yule mvulana aliyeuliza darasa litaanza lini akainuka na kuanza kurukaruka juu na chini, huku akipiga makofi.
“Jumping jacks! Huko sasa ni ubunifu!”
“Ah, na hili hapa ni jambo la kufurahisha hasa. Mkimaliza mwendo usiokoma, mnaweza kuketi, kusimama, kulala tena, kadhalika, kadhalika.”
“Ni kama mzunguko. Sehemu ya raha ni kwamba nyinyi ndio mnaoamua. Mpira uko kwenu. Mnaelewa?”
Wanafunzi wote wakaitikia kwa vichwa kwa shauku kubwa.
“Lakini nitajuaje wakati wa kuacha?” akauliza yule msichana mwenye nywele nyekundu, maneno yakimtoka kwa shida katikati ya mizunguko ya nyonga zake.
“Hiyo ndiyo sehemu bora kuliko zote,” akatangaza mwalimu kwa mbwembwe.
“Unajua tu.
Utajua tu!”
A story by Pemba Umoja