Mwanamfalme Mpole

Ngano ya Tahadhari ya Urithi

Mwanamfalme Mpole — a story by Pemba Umoja

Mwanamfalme mpole alikuwa wa mwisho kuzaliwa, akiwa na dada watatu wakubwa — daima alidekezwa, lakini daima alikuwa safi moyoni.

Dada zake walijisifu kuhusu vito vyao, magauni yao, na nyumba zao za wanasesere.

Lakini mwanamfalme mpole alivaa nguo zilizochanika, akachezea ala za zamani zilizoachwa katika uwanja wa mchanga wa kasri.

Alikua mnyenyekevu, na mwenye fadhili.

Dada zake daima walikuwa na shauku kuhusu binamu zao.

Nani alikuwa mrembo zaidi? Mwembamba zaidi? Tajiri zaidi?

Nani aliolewa na nani?

Walikuwa warembo kiasi gani, wembamba kiasi gani, na matajiri kiasi gani?

Siku moja wazazi wa mwanamfalme mpole walifariki dunia.

Dada zake walimgeukia kwa shingo upande na kumpa funguo za kasri.

Alivaa joho la hariri la baba yake, medali ya zumaridi ya mama yake iliyokuwa na ukubwa wa ngumi, akatia soksi zake zenye matundu katika viatu vya ngozi ya ndama, kisha akawakodolea macho dada zake.

Alikodolea macho kasri yake.

Aliwakodolea macho raia zake.

Alizikodolea macho ardhi zake zisizo na mwisho.

“Nani tajiri kuliko wote katika nchi hii?” aliuliza. “Nani?” akaamrisha.

Dada zake wakatazamana, wakimtambua ndugu yao kwa shida.

“Wewe. Ni wewe,” walijibu kwa woga.

Ndugu yao alicheka. Akapiga fundo la asali ya pombe. Kisha lingine.

Alikula mapaja ya mwanakondoo na bata mzinga kwa ulafi, akijifuta mdomo kwa mkono wa joho lake la hariri. Tabasamu hafifu likatokea kwenye midomo yake.

“Ndiyo mimi. Ndiyo mimi,” alirudia.

A story by Pemba Umoja