Kuacha Kundi

Nini Hutokea Unapopata Taswira ya Ulimwengu Mwingine

Kuacha Kundi — a story by Pemba Umoja

Ilikuwa raha sana kucheza na kundi. Kila siku jua ling'ara na tungeenda kula mayai kutoka kwenye miamba.

Siku moja, maji yote mbele yetu yalifunikwa na umbo geni lililofura na maji yakachafuka kama kuna dhoruba kuu.

Kiumbe cha ajabu kilitokea pasipojulikana kikiwa kimeshika chakula cha kupendeza kwa njia ya kushangaza. Ilionekana kana kwamba kinatoka juu—kutoka ulimwengu mwingine.

Kiumbe hicho kilivunja-vunja chakula hiki cha ajabu na kukifanya vipande vidogo, vitamu. Ilikuwa ni ladha ambayo sikuwahi kuionja kamwe. Bora kuliko yale mayai tuliyokula kila siku.

Sote tulikimbilia kwa fujo ili kunyakua kiasi kikubwa tuwezacho.

Viungo virefu, vya ajabu vya kiumbe huyo vilishikilia matonge hayo kati ya viganja vyake vilivyo kama koleo.

Na hapo ndipo lilipokuwepo. Donge kubwa na nono kuliko yote, katikati ya koleo ndefu, nyembamba.

Niliogelea kwa kasi, kwa ukali, ili kulidai tonge hilo liwe langu.

Ghafla, vile viganja vya ajabu vilinikamata. Nilinaswa, kisha nikainuliwa juu mbinguni. Sikuweza tena kupumua. Sikuona vizuri. Nilikuwa peke yangu.

Ngozi yangu ilianza kuwasha. Kulikuwa na nuru kali.

Nilijinyonga-nyonga na kujinyonga-nyonga na kujinyonga-nyonga nikijaribu kwa nguvu zangu zote kujinasua kutoka kwenye mshiko wa kiumbe huyo.

Na katika muda ambao utabaki daima umenakshiwa akilini mwangu, nilitoroka kutoka kwenye koleo zilizokaza, nikaanguka kwenye ombwe. Yote yalikuwa kama ukungu. Na kisha nikajikuta niko miongoni mwa kundi tena. Walikuwa njiani kwenda kula mayai kwenye miamba.

Niliungana nao kwa furaha.

Sikutaka kamwe kujaribu tena vyakula vya kigeni. Sikutaka kamwe kuliona lile umbo lililofura lililoleta dhoruba katika ulimwengu wetu. Nilijiahidi kwamba ningeenda mbali, mbali sana ikiwa ningeziona tena koleo za kile kiumbe cha ajabu.

Lakini kile chakula? Je, nitakisahau kamwe?

Kundi liliniuliza kama nilikuwa salama. Sikuwa na uhakika.

Nilikuwa nimeenda wapi? Je, nilikuwa nimemwona Mungu? Kiumbe kutoka sayari nyingine?

Wengine walianza kunitendea tofauti. Hata kuniheshimu. Nilikuwa nimekwenda juu.

Walikuwa wameniona nikiuacha ulimwengu wetu na kurejea.

Nilitamani kuwa kama wao tena, lakini sikuweza kamwe.

Macho yangu yalikuwa yamefunguliwa kuuona ulimwengu mpya kabisa.

Ningekuwa tofauti daima.

A story by Pemba Umoja