Jasper Wingu Juu ya Kiribati
Wingu Lililojifunza Kubadili Umbo, na Kisiwa Alichokiangalia
Jasper alikuwa wingu. Aliishi juu ya Tarawa katika nchi ya Kiribati, inayotamkwa Kiribas.
Jasper alikuwa na umri mkubwa kuliko mawingu mengi, ambayo yana umri wa masaa mawili hadi kumi tu. Jasper alikuwa na umri wa miaka 500.
Wingu linawezaje kuwa na umri mkubwa hivyo? unauliza.
Jasper alijifunza sanaa ya kugeuzwa sura.
Naam, kugeuzwa sura. Ni kweli, hilo ni neno la vitabuni hasa. Siyo mimi peke yangu ninayejaribu kukuvutia.
Kugeuzwa sura, kulingana na Kamusi ya Bahari ya Pasifiki, takriban 1405, ni ubadilishaji wa maumbo kutoka umbo moja hadi jingine.
Je, umewahi kuona mamba angani?
Wakati mwingine Jasper alijigeuza kuwa mmoja. Alifurahia pindi fulani kuwatisha watoto, lakini ni watu wazima ndio waliokuwa wakiogopa zaidi, hasa wale waliojifanya wagumu.
Jasper alikuwa na macho makali. Aliweza kuwaona wakijikunja kwa wasiwasi, hasa alipofungua taya zake kubwa na kuonyesha meno yake makali yasiyo na mpangilio.
Lakini kwa kugeuzwa sura, Jasper alibadilisha umbo tena na kuwa ua zuri la msibu. Masibu yalikuwa maua aliyoyapenda zaidi. Yalikuwa na harufu nzuri, laiti Jasper angeweza kunusa.
Alipenda jinsi watoto walivyotazama masibu na kwenda kuyatafuta walipoyaona angani.
Watoto hawakupitwa na lolote. Ni watu wazima ndio ambao walikuwa hawaoni.
Siku moja mamba. Siku moja msibu.
Jasper aliweza kubadilika na kuwa chochote alichotaka.
Baada ya muda Jasper alianza kuwa na wasiwasi. Kiribati ilikuwa inazidi kuwa ndogo zaidi na zaidi. Bahari ilikuwa inazidi kuwa kubwa zaidi na zaidi.
Watu ilibidi wahamishe nyumba zao nyuma zaidi. Walipanda mikoko, miti yenye mizizi mirefu, ili kushikilia mchanga pamoja.
Lakini kadiri miaka ilivyopita kisiwa kilizidi kuwa kidogo zaidi na zaidi, na bahari ikazidi kuwa kubwa zaidi na zaidi.
Jasper alibadilika na kuwa mweusi na wa zambarau. Alilia mvua nyingi sana. Alikuwa na huzuni kubwa.
Watoto walikuwa na ufukwe mdogo wa kuchezea.
Baada ya muda watu walianza kuondoka kwa boti na ndege.
Jasper alijaribu kujigeuza umbo la nyumba ili kuwatumia watu wa Kiribati ujumbe kwamba wabaki.
Jasper hakutaka waondoke.
Miaka ikapita. Bahari ikazidi kuwa kubwa. Punde si punde watu wote walikuwa wameondoka.
Jasper alibaki.
Jasper alijigeuza umbo la watoto wa Kiribati, lakini walikuwa wameondoka. Ni samaki wanaoruka pekee ndio waliotazama.
Jasper alizidi kuwa mweusi na wa zambarau. Akanyesha na kunyesha na kunyesha.
Jasper hangeweza kuwasahau kamwe watoto wa Kiribati.
Alitumaini popote walipoenda, wangezungukwa na masibu.
A story by Pemba Umoja