Bomba la Maji
Mtaa wa Jiji Uliojaa Watu
Familia ya Jacobs ilienda matembezini mashambani. Waliishi kwenye mtaa wa jiji uliojaa watu. Nyumba zote zilikuwa zimeungana na zilionekana kama maghala makubwa ya nafaka yaliyojaza vitalu baada ya vitalu.
Waliporudi waliona gari maridadi aina ya SUV likizuia bomba la maji la kuzimia moto.
Bwana Jacobs alikuwa anataka kupigia simu mamlaka ya jiji. Alikuwa na wasiwasi kidogo kwamba kikosi cha zimamoto hakingeweza kulifikia iwapo kungetokea dharura.
“Nadhani nitapigia simu mamlaka ya jiji,” alipendekeza.
“Usithubutu,” mkewe alimkemea. “Hao ni majirani zetu. Wanaishi ng’ambo ya barabara.”
“Ni yule daktari mchangamfu mwenye kigari cha mtoto,” mwanawe alisema.
“Hapana, si yeye,” Bwana Jacobs alijibu. “Wana gari tofauti.”
Hata hivyo, Bwana Jacobs aliamua kutopigia simu mamlaka ya jiji. Hakuweza kustahimili joto kutoka kwa familia yake.
Familia ya Sanchez ilipanga fleti kwenye ghorofa ya tatu ya jengo lililopakana na nyumba ya familia ya Jacobs.
Bi. Sanchez alikuwa safarini kikazi. Bwana Sanchez alikuwa anataka kuandaa chipsi za viazi vitamu alizozipenda sana. Bi. Sanchez hakuruhusu hilo kamwe alipokuwa nyumbani. Hakupenda mafuta kurukia kila mahali.
Chipsi za viazi vitamu zilikuwa jikoni zikipikwa wakati Bwana Sanchez alipopokea simu kutoka kwa mwajiri wake kuhusu tatizo la sakafu ya paa karibu na hapo. Aliangalia simu yake ili kupitia michoro.
Wakati huohuo mafuta yaliyokuwa yakiruka yalishika moto, yakaliwasha jiko. Bwana Sanchez aliachia simu yake ikaanguka na kutafuta kizima-moto. Hakukumbuka kilikuwa wapi. Moto ulienea kwa ukali juu ya meza ya jikoni, ukiiteketeza nguo nyeupe ya meza. Kila kitu kilionekana kwenda polepole huku makaa yaliyowaka na moshi vikijaa hewani.
Bwana Sanchez alimnyakua Kitty kutoka kwenye kochi na kukimbilia nje. Miali ya moto iliimeza ghorofa ya nne ya jengo hilo kisha ikacheza hadi kwenye majengo yote mawili yaliyopakana nalo.
Bwana Jacobs alikuwa akioga kwenye bafu la mvua. Alisikia mayowe hafifu kupitia mvuke. Ilionekana kuna kitu kingine mbali na mvuke kilichokuwa kikizunguka beseni la kuogea.
Alifunga maji na kuugusa mlango wa bafu. Ulikuwa na joto kali la kuunguza. Moshi ulitawala mahali pa mvuke.
Alitweta akitafuta pumzi. Aliwasha tena bafu la mvua. Dari iliporomoka ndani ya beseni la kuogea.
Magari ya zimamoto yalizunguka mtaani. Hayakuweza kulifikia bomba la maji la kuzimia moto.
Bwana Jacobs hakuweza kustahimili joto tena wakati beseni la kuogea lilipoporomoka kutoka chini yake.
A story by Pemba Umoja